Matokeo ya Uhakiki wa Udahili awamu ya pili.
TAARIFA KWA UMMA
MATOKEO YA UHAKIKI WA UDAHILI AWAMU YA PILI KWENYE PROGRAMU MBALIMBALI KATIKA MKUPUO WA SEPTEMBA 2022/2023
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) linapenda kuutaarifu umma kuwa uhakiki wa sifa za waombaji wa udahili waliowasilishwa na Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa awamu ya pili kwa ajili ya Mwaka wa Masomo 2022/2023 umekamilika. Na kwamba matokeo ya uhakiki wa sifa za udahili yametumwa kwa Vyuo husika leo tarehe 31Oktoba, 2022.
Hivyo, waombaji wa kozi za Astashahada na Stashahada waliotuma maombi ya kudahiliwa katika Vyuo hivyo wanaweza kufuatilia hali za udahili wao. Katika awamu hii, jumla ya Vyuo 237 viliwasilisha waombaji 25,530 waliochaguliwa kujiunga na programu mbalimbali kwa ajili ya uhakiki. Kati ya hao, waombaji 24,234 (94.9%) ambapo wanawake 13,404 (55.3%) na wanaume 10,830 (44.7%) wamekidhi vigezo vya kujiunga na programu mbalimbali walizochagua.
Aidha, jumla ya waombaji 1,296 (5.1%) sawa na wanawake 693 (2.7%) na wanaume 603 (2.4%) hawakuwa na sifa za kujiunga na programu walizoomba. Baadhi ya Vyuo viliwasilisha waombaji 120 (0.5%) bila ya taarifa zao kwa ajili ya Baraza kujiridhisha kama wanazo sifa za kujiunga na programu husika. Majina ya waombaji waliohakikiwa tayari yametumwa Vyuoni ili waweze kuwapa taarifa waombaji wao.
Pia, waombaji wote waliowasilishwa kwa ajili ya uhakiki wanaweza kufuatilia hali zao za udahili kwenye Vyuo walivyoomba kwa kutumia msimbo (code) waliotumiwa kupitia simu na barua pepe zao zilizowasilishwa na Vyuo kwa kubofya kitufe cha “Verificationresults 2022” katika tovuti ya NACTVET (www.nacte.go.tz).
Baraza linasisitiza wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhakikisha kwamba wamesajiliwa kwenye mfumo wa Baraza na Vyuo vyao kabla ya tarehe 18 Novemba, 2022.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA KATIBU MTENDAJI
BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI NA MAFUNZO YA UFUNDI STADI (NACTVET)
31/10/2022